Sonona kwa watu wazima
Depression in adults
Angalizo
Tazama kanusho letu, ambalo linatumika kwa tafsiri zote zinazopatikana kwenye tovuti hii.
Kuna tofauti gani kati ya kujisikia mtu duni na mwenye sonona?
Kuna wakati kila mtu katika maisha yake anajisikia kuchoshwa au mwenye taabu. Mara nyingi huwa ni kwasababu maalum, haiingilii sana maisha ya kila siku na kawaida haiendelei zaidi ya wiki moja au mbili.
Hata hivyo, hisia hizi zikiendelea kwa wiki kadhaa au miezi kadhaa, au ikawa mbaya na kuanza kuathiri maisha ya kila siku, unaweza ukawa na sonona na unahitaji kutafuta msaada.
Zipi ni dalili za Sonona
Watu wanakuwa na viwango tofauti vya sonona kwa njia tofauti. Kuna kiwango kidogo, cha wastani na kikali.
Hali ya Sonona ya watu pia inachangiwa na utamaduni wao na madili yao, imani na lugha.
Ukiwa na sonona utagundua baadhi ya haya yafuatayo:
Kiakili
- Kujisikia kukosa raha, mwenye taabu, uko chini, mnyonge- hii hali haiondoki na inakuwa mbaya zaidi wakati fulani wa siku, mara nyingi pale tu unapoamka
- Huwezi kufurahia chochote
- Unapoteza hamu ya kuonana na watu na unapoteza mguso na marafiki
- Hauko makini na unapata ugumu kufanya maamuzi
- Hujiamini
- Unahisi ni mwenye hatia na usiyestahili
- Unaamini mambo yatakuwa mabaya zaidi
- Unahisi kukosa matumaini, na labda hata kujiua
Kimwili unaweza ukahisi:
- unakosa utulivu,una woga au unakasirika
- unachoka na huna nguvu
- Hupati usingizi au unapata usingizi mwingi
- Unaamka mapema sana asubuhi na/au unakaa macho usiku kucha
- Unaumwa kichwa au tumbo linachafuka
- Unapoteza hamu na ngono
- Huwezi kula chakula na unapoteza uzito au unazidisha kula kujifariji na unaongeza uzito
Watu wengine wanweza kugundua kuwa:
- unafanya makosa kazini au unakuwa huna malengo
- Uko mkimya kuliko kawaida na umejitenga, unakaa mbali na watu
- Una wasiwasi kuhusu vitu kuliko kawaida
- Unahamaki au una hasira kuliko kawaida
- Unala usingizi zaidi au usingizi mchache/kidogo kuliko kawaida
- Unalalamika kuhusu matatizo ya mwili yasiyoeleweka
- Umeacha kujitunza vizuri- huoshi nywele au nguo
- Umeacha kutunza nyumba yako vizuri- umeacha kupika, husafishi au unasahau kubadili mashuka kwenye kitanda
Watu wengi hawapati dalili hizi, na baadhi ya watu wanaweza tu kuona dalili za mwili. Unaweza kufikiri una matatizo ya afya ya mwili kwasababu unajisikia mchovu au una matatizo ya usingizi, lakini dalili za mwili kama hizi zinaweza kuwa kiashiria cha kwanza cha sonona
Unaweza usigundue ulivyosononeka, hasa kama hali hii inajitokeza taratibu. Wakati mwingine watu wanajaribu kujisukuma na kujilaumu kuwa ni wavivu au hawana uwezo wa kufanya chochote
Wakati mwingine inachukua rafiki au mwenza kukushawishi kwamba kweli kuna tatizo na kushauri utafute msaada.
Unaweza kuomba msaada kama rafiki au mwenza akiona kuwa:
Hisia zako za sonona zinaathiri kazi yako, maslahi yako, na hisia zako kwa wanafamilia au marafiki.
Hisia zako za sonona zimekuwepo kwa muda na hakuna dalili unapata nafuu.
Unajikuta unahisia maisha hayana thamani, au watu wengine watakuwa na nafuu bila wewe.
Vipi kuhusu hali ya wasiwasi?
Baadhi ya watu wanaweza pia kuwa na wasiwasi wakiwa na sonona
Unaweza kujisikia uko ukingoni wakati wote, mwenye woga, mwenye hofu na unaona ugumukutoka nje au kuwa miongoni mwa watu. Au, unaweza kupata dalili za mwili kwama vile mdomo kuwa mkavu, kutokwa na jasho, kukosa pumzi au tumbo kuvurugika.
Kama ukipata dalili za sonona na wasiwasi, kwa kawaida utapewa tiba ya mojawapo linaloleta matatizo zaidi.
Vipi kuhusu bipolar disorder (manic depression)?
Baadhi ya watu wenye sonona wanaweza pia kuwa na vipindi virefu vya kujisikia mwenye furaha ya kupindukia/ya kupitiliza na msisimko kupita kiasi. Hii hali inaitwa ‘Mania’ na inaweza kumaanisha unaweza ukawa na ugonjwa wa ‘Bipolar disorder’ (zamani ulikuwa unaitwa Manic depression).
Tafadhali angalia taarifa zetu kuhusu ugonjwa wa hisia kutafuta ni wakati gani na ni kwa namna gani utapata msaada kama unafikiri una hali hii
Ni kwanini sonona inatokea?
Sonona sio ishara ya udhaifu. Inaweza kutokea hata kwa wale wenye dhamira- hata watu maarufu, wanariadha, na watu mashuhuri wanaweza kupata sonona.
Kuna wakati kuna sababu ya wazi kabisa ya kuwa na sonona, wakati mwingine hakuna. Inaweza kukatisha tamaa, kuchanganyikiwa au kwasababu umepoteza kitu au mtu muhimu kwako.
Mara nyingi kuna sababu zaidi ya moja, na hizi zitakuwa tofauti kwa watu tofauti. Tutaelezea sababu za kawaida hapa chini.
Matukio ya maisha na hali ya mtu
Sonona inaweza kuletwa na tukio lenye kuleta msongo wa mawazo lenye kuhuzunisha kama vile kufiwa, uhusiano unapovunjika au kupoteza kazi.
Kama matukio ya maisha inamaana unaishi mwenyewe au huna marafiki au familia, kuna uwezekano wa kupata sonona.
Afya ya mwili
Usingizi, chakula na mazoezi vyote vinaweza kuathiri hali (mood) na jinsi tunavyo kabiliana na mambo.
Matatizo ya afya ya mwili, hasa yale makubwa au ya muda mrefu, yanaweza kusababisha sonona au kufanya uwe mbaya zaidi.
- Magonjwa yenye kuhatarisha maisha kama kansa na magonjwa ya moyo
- Magonjwa ya muda mrefu na/au ya mauvmivu kama magonjwa ya yabisi- kavu
- Magonjwa yanayotokana na virusi kama mafua makali au homa ya tezi hasa kwa vijana
- Matatizo ya homoni, tezi ya dundumio isiyofanya kazi vizuri
- Matatizo yanayoathiri ubongo au mfumo wa neva.
Kupitia matukio mabaya utotoni
Kuna baadhi ya watu wako kwenye hatari zaidi ya kupata sonona kupita wengine. Hii inaweza kuwa kwasababu walipitia matukio mabaya utotoni au walipata pamoja na unyanyasaji wa (kimwili, kijinsia au kisaikolojia), kutelekezwa, kushuhudia vurugu au tukio baya, au familia isiyo na mazingira imara.
Pombe na matumizi ya madawa ya kulevya
Unywaji wa pombe kupindukia au kutumia madawa ya kulevya kama bangi inaweza kukufanya uwe na uwezekano mkubwa wa kuwa na sonona baada ya muda mrefu.
Kwa taarifa zaidi anagalia kipeperushi kuhusu pombe na sonona
Sababu za kinasaba
Vinasaba vinavyofanana vya ‘sababu hatarishi’ vinahusika kwenye mtu fulani kupata sonona, ugonjwa wa hisia au skizofrenia. Pia kuna sababu hatarishi za mazingira, na hizi zinaweza kuingiliana na sababu hatarishi za kinasaba kuongeza au kupunguza uhatarishi wako wa kupata hali hizi/magonjwa haya.
Kwa mfano, unaweza ukawa na kinasaba hatarishi ambayo inamaanisha una uwezo mkubwa kupata sonona kali. Hata hivyo, kama umekulia au umeishi kwenye mazingira imara na chanya hii inaweza kupunguza uhatarishi wa kupata ugonjwa mkali wa akili.
Kuwa na wazazi wenye magonjwa makubwa ya akili kama sonona ni sababu hatari yenye nguvu inayojulikana kufanya upate magonjwa makubwa ya akili. Watoto wenye mzazi ambaye ana ugonjwa mkubwa wa akili ana nafasi 1 kati ya 3 ya kupata ugonjwa mkubwa wa akili.
Unapofikiria kuhusu sababu za kupata sonona, ni muhimu kukumbuka kuwa kuna vitu vingi sana vinahusika na sio sbabub moja tu hatarishi inasababisha sonona.
Je sonona inatofautiana jinsia na ujinsia vinapohusishwa?
Wanaume ambao wanapata sonona ni mara chache wanazungumzia hisia zao na ni mara chache wanaomba msaada. Sonona wao unajionyesha namna tofauti, kupitia hasira, kupoteza udhibiti, kufanya vitu vya hatari kubwa na ushambulizi, vile vile utumiaji wa pombe na madawa ya kuevya kukabiliana na hali hiyo.
Kadiri ya asilimia 12 ya wanawake walio waja wazito watapata sonona wakati wa uja uzito wao, wakati asilimia 15 hadi 20 watapata sonona ndani ya mwaka mmoja baada ya kuzaa.
Kwa taarifa zaidi, tafathali angalia kipeperushi chetu kuhusu Sonona baada ya kuzaa. (Postnatal depression).
Watu waliobadili jinsia (wanajitambulisha kwa jinsia tofauti na jinsia yao wakati wanazaliwa) anaweza kupata sonona wa hali ya juu na wasiwasi uliopitiliza kuliko wale wanaojitambulisha kwa jinsia yao wakati wanazaliwa. Watu ambao hawajitambulishi jinsia yao (hawajitambulishi kama ni mke/wa kike au mme/wa kiume) wanaweza pia wakawa na sonona kali na wasiwasi uliopitiliza.
Watu ambao utambulisho wao ni msagaji, shoga au wa jinsia mbili wana uwezekano mkubwa kupata matatizo ya afya ya akili (pamoja na sonona) kuliko wale wa jinsia moja. Pia wanauwezekano mkubwa zaidi wa uhatarishi wa kujaribu kujiua na kujiumiza.
Je, ninaweza kupata nafuu mwenyewe?
Habari nzuri ni kuwa watu wengi wenye sonona watapata unafuu kwa kufanya vitu vya kujisaidia wenyewe. Unaeza kuushinda sonona mwenyewe, amabpo utapata hisia za mafanikio na kujiamini kukabiliana na hisia hizo tena kama ukujisikia hisia ziko chini siku zijazo.
Ukichukua baadhi ya mapendekezo kwenye kipeperushi hiki unaweza kufupisha kipindi cha sonona na inaweza kukusaidia kujisikia nafuu siku zijazo.
Lakini kuna baadhi ya watu wanahitaji msaada zaidi, hususan kama sonona wao ni mkali sana au unaendelea kwa muda mrefu, au baadhi ya vitu walivyotumia kupata unafuu havijafanya kazi.
Kama ni mara ya kwanza kupata sonona, takribani una nafasi 50 kwa 50 ya kupata sonona tena, kwahiyo ni muhimu kujua jinsi ya kupata msaada pale unapouhitaji.
Kwahiyo ukifikiri unahitaji msaada wa kuongea na mtu kuhusu hisisa zako, jitahidi usiache kufanya hivyo, kwakuwa inaweza kusaidia wewe kurudia kufanya vitu ulivyozoea na kufurahia maisha mapema zaidi.
Wakati mwingine inaweza kuhtaji kurudia mara kadhaa kuwafanya watu wengine waelewe hisia zako. Endelea na usikate tamaa- unaweza kupata msaada sahihi.
Ninawezaje kujisaidia mwenyewe
Hizi ni baadhi ya mapendekezo unayoweza kujaribu unapojisikia una sonona. Ni muhimu kuwa unatafuta lipi linakufaa wewe na kutengeneza orodha ya mikakati inayosaidia.
Ongea na mtu: Kama umepata habari mbaya au mshtuko mkubwa katika maisha, jaribu kutoficha hisia zako. Inaweza kusaidia unapomuambia mtu wa karibu jinsi wewe unavyojisikia kuhusu habari hiyo au mshtuko huo. Kama unaona huwezi kuongea na mtu yeyote, jaribu kuandika jinsi unavyojisikia.
Endelea kujishughulisha: Kama unaweza, toka nje na ufanye mazoezi kiasi, hata kama ni kutembea umbali mfupi. Hii itakusaidia kufanya mwili uwe sawa (fit) na ulale vizuri zaidi. Inaweza pia kukusaidia kuzingatia vitu vingine na sio kuwa mwenye mawazo au hisia za uchungu.
Kula vizuri: Unaweza ukawa husikii njaa sana, lakini jaribu kula mara kwa mara. Ni rahisi kupoteza uzito au kupungukiwa vitamini ukiwa na sonona- au kula vyakula vilivyokwisha pikwa au vya kwenye paketi na kuongeza uzito ambao huutaki. Lishe bora, na matunda na mboga kwa wingi, vinaweza kufanya mwili wako na akili viwe vyenye afya.
Epuka pombe na madawa ya kulevya: Pombe inaweza kukufanya ujisikie vizuri kwa masaa machache, lakini kwa ukweli ni kwamba inakufanya uwe na sonona kali hapo mbeleni. Hii ni sawa na madawa ya kulevya, hasa bangi, amfetamini (Amfetamine), kokeni (Cocaine), ekstasi (Ecstacy).
Tengeneza utaratibu wa kulala: Jaribu Kwenda kulala muda ule ule kila usiku na uamke muda ule ule kila asubuhi. Fanya kazi yenye kupumzisha unayoifurahia kabla hujaenda kulala, kama kusikiliza muziki au kusoma kitabu. Kama huwezi kulala, toka kitandani na ufanye kitu cha kupumzisha kama kuketi kimya kwenye kochi.
Kwa taarifa zaidi kuhusu kulala, angalia kipeperushi cha kulala vizuri
Jaribu shughuli za kupumzisha: Kama mwili umekakamaa kila wakati, jaribu kufanya mazoezi ya kupumzisha, yoga, masaji, aromatherapy, au shughuli nyingine itakayokupumzisha.
Fanya kitu kinachokufurahisha: Chukua muda mara kwa mara wa kufanya kitu ambacho hakika kinakufurahisha- kama kucheza michezo, kusoma, au kitu kingine upendacho kufanya.
Soma kuhusu sonona: Kuna vitabu vingi na tovuti nyingi kuhusu sonona. Vinaweza kusaidia kukuelewesha kinachoendelea, kukupa mikakati ya kukabiliana vizuri zaidi, na pia kuwasaidia marafiki na ndugu zako kuelewa unachokipitia.
Fanya zoezi la ukarimu-binafsi: Inawezekana wewe ni mtu unayependa ukamilifu (perfectionist) unayejisukuma kupita kiasi. Jaribu kujiwekea malengo au matarajio halisi. Uwe mkarimu kwako mwenyewe.
Pumzika: Inaweza ikasaidia sana ukaenda mahali na nje ya utaratibu wako wa kawaida kwa siku chache. Jipe mapumziko kutoka kwenye msongo wa mawazo wa kila siku au wasiwasi. Ukiweza kubadili mazingira, hata kwa masaa machache, inaweza kusaidia.
Jiunge na kikundi cha kusaidiana: Inaweza kuwa vigumu kujisaidia ukiwa na sonona. Kuongea na watu wengine walio katika hali kama yako inaweza kusaidia. Angalia orodha ya mashirika mwisho wa kipeperushi hiki kupata baadhi ya mawazo.
Kuwa na imani
Jikumbushe kuwa watu wengi wamewahi kupata sonona na wakapata nafuu-msaada unapatikana na unastahili kupata msaada unaohitaji kukufanya upate nafuu.
Naweza kupata msaada gani kwa sonona
Kama ulipojaribu kupata nafuu mwenyewe hukufanikiwa kama ambavyo ungependa au kwa haraka unavyotaka, basi inaweza kuwa wazo zuri kuongea na daktari wako (Gp).
Watu wengi wenye sonona wanatibiwa na madaktari wao. Kama huna daktari anayekuona mara kwa mara, jaribu kutafuta daktari maeneo hayo ambaye utajisikia vizuri kumuona mara kwa mara.
Daktari wako ataongea na wewe na kupitia dalili zako na kutafuta ni tiba ipi itakusaidia.
Tiba bora itategemea na kiwango cha sasa cha sonona, umedumu kwa muda gani, na kama umewahi kuwa na sonona zamani.
Daktari wako anaweza pia kukufanyia uchunguzi wa kina wa mwili. Hii ni kwasababu kuna baadhi ya magonjwa ya mwili yanaweza kusababisha sonona. Kama tayari unapata matibabu ya ugonjwa wa mwili, daktari wako atahitaji kujua kuhusu hilo.
Tiba ya awali (Sonona kidogo)
Kama ni mara ya kwanza kupata sonona, kwa kawaida hutapewa dawa za sonona. Daktari wako anaweza kushauri tiba ya kisaikolojia ya kina cha chini (au tiba kwa kutumia mazungumzo) kama vile:
- Vipeperushi vya kujisaidia mwenyewe inayohusisha Cognitive behavioural therapy (CBT) principles (ukisaidiwa na mtaalamu wa afya)
- Programu ya kompyuta ya CBT ya kujisaidia mwenyewe (pia ukisaidiwa na mataalamu wa afya)
- Mazoezi ya kutumia vikundi
- Programu ya maozezi ya vikundi, ama yanahusisha kujisaidia kutumia msaada kutoka kwa wanakikundi wenzako au CBT
Daktari wako atakusaidia kuchagua tiba itakayokufaa.
Kama tiba hizi hatizafanya kazi, daktari wako atashauri moja ya tiba kati ya zifuatazo za kutibu sonona ya wastani na kali.
Tiba zingine (Sonona wastani na sonona kali)
Daktari wako anaweza kushauri tiba ya kisaikolojia ya kina cha juu au dawa za sonona au tiba zote mbili. Unaweza kuongea nae kuamua tiba ipi itakufaa zaidi.
Tiba za kisaikolojia
Kuna aina nyingi za tiba za kisaikolojia kwa wale wenye sonona na unaweza kuelekezwa uende kuhudumiwe na kupewa yoyote iliyopo maenea ya karibu na unapoishi.
Kama kuna orodha ya wanaosubiri kabla ya kupata aina fulani ya tiba ya kisaikolojia, unatakiwa uongee na daktari wako kuhusu nini cha kufanya kujitunza wakati unasubiri.
Cognitive behavioural therapy (CBT)
Wengi wetu tuna tabia ya kuwa na fikra hasi ambazo, ukiacha yanayotokea maishani, zinaweza kwa kiasi Fulani kutufanya tuwe na sonona na tuendelee kuwa nayo.
CBT inaweza kusaidia:
Kugundua fikra zisizo za kweli au zisizosaidia halafu upate, njia mpya na zinazosaidia zaidi ufikiriaji na utendaji.
CBT imeshuhudiwa zaidi kama tiba ya sonona.
Angalia kipeperushi chetu kuhusu Cognitive behavioural therapy kwa taarifa zaidi.
Interpersonal therapy (IPT)
Interpersonal therapy inaweza kukusaidia kugundua na kushughulikia tatizo lolote linalohusu mahusiano yako na familia, washirika wako na marafiki.
Behavioural Activation
Behavioural activation inakuhimiza uendeleze zaidi tabia chanya kama vile kupanga shughuli na kufanya vitu vya kujijenga ambavyo ulikuwa unakwepa kuvifanya.
Couples therapy
Kama uko kwenye uhusiano unaoonekana kuathiri sonona yako, basi couples therapy inaweza kuwa tiba sahihi kukusaidia kuelewa vinavyounganisha sonona na uhusiano. Inaweza kusaidia kujenga uhusiano imara zaidi kati yako na mwenzako.
Ushauri
Washauri waliopata mafunzo wanaweza kukusaidia kutafiti dalili na matatizo yako, na wakakupatia msaada na maelekezo.
Psychodynamic psychotherapy
Tiba hii inakusaidia kuona jinsi matukio ya zamani yanavyoweza kuathiri maisha yako ya sasa.
Dawa za sonona
Kama sonona yako ni ya wastani au kali au inaendelea kwa muda mrefu, daktari wako anaweza kushauri utumie dawa za sonona, mara nyingi ile ya aina ya Selective serotonin reuptake inhibitor (SSRI). Watazungumza na wewe kuhusu ipi itakuwa inafanya kazi vizuri zaidi kwako- hii itategemea kama umeshawahi kutumia dawa ya sonona zamani, kama unatumia dawa zingine, na matatizo mengine yoyote ya afya ya mwili uliyonayo.
Je, dawa za sonona zina madhara?
Kama dawa nyingine zote, dawa za sonona zina madhara, japokuwa huwa ni kidogo na huwa yanaisha baada ya kama wiki mbili.
Daktari wako atakushauri cha kutegemea na unashauriwa kuongea nae kama kitu chochote kinakutia wasiwasi, au utapata madhara yoyote. Utapewa pia taarifa ya kimaandishi kutoka kwa mfamasia wako.
Kama dawa ya sonona inakufanya usinzie, unatakiwa uitumie usiku, ili ikusaidie kulala.Ila, kama unasinzia mchana, usiendeshe gari au kufanya kazi za kutumia mashine mpaka hii hali iishe. Pombe inaweza kukufanya usinzie zaidi kama ukinywa wakati unatumia dawa, kwahiyo ni bora usinywe.
Mbali na baadhi ya dawa zingine na madawa (kama vile nikotini (nicotine) au pombe), hutajikuta unatamani dawa za sonona, au kujisikia kama unahitaji kutumia nyingi zaidi kupata unafuu ule ule.
Ni kwa muda gani nitahitaji kutumia dawa ya sonona?
Mwanzoni, daktari wako atahitaji kukuona mara kwa mara (baada ya wiki 2, halafu kati ya wiki 2-4 kwa miezi mitatu ya kwanza, halafu mara chache) kuhakikisha kuwa tiba inafanya kazi.
Kama ulikuwa na fikra za kujiua, au una umri chini ya miaka 30, daktari wako anaweza kukuona mara nyingi zaidi (kawaida kila wiki). Hii ni kwasababu baadhi ya dawa za sonona zinaweza mwanzoni kuongeza fikra za kutaka kujiua, hasa kama bado kijana.
Kama kutumia dawa za sonona kunasaidia, unatakiwa kutumia sio chini ya miezi 6, hata kama unajisikia vizuri. Hii inaweza kusaidia kupunguza uwezekano wa sonona kurudi.
Unaweza kuendelea nazo kwa muda mrefu zaidi ya huo kama umewahi kupata sonona zamani. Daktari wako atakushauri lini uache kutumia na jinsi ya kuacha kwa usalama.
Kama utaacha kutumia dawa za sonona ghafla, unaweza kupata dalili zitokanazo na kuondoa dawa. Hivi zinaweza kuwa matatizo ya usingizi, wasiwasi, kizunguzungu au maumivu ya tumbo.
Kama unafikiri dawa ya sonona haifanyi kazi (baada ya kutumia kwa wiki 2 au 4), basi ongea na daktari wako, ambaye anaweza kubadilisha kiasi cha dawa unachotumia au kukupa aina nyingine ya dawa ya sonona.
Kupata msaada zaidi (Sonona kali)
Watu wengi wenye sonona wanapata msaada wanohitaji kutoka kwa madakatari wao. Kama sonona yako haipati nafuu baada ya kupewa tiba kupitia kwa daktari wako na unahitaji msaada zaidi wa kitaalamu, unaweza kupelekwa kwenye idara au timu inayotoa huduma za afya ya akili.
Mtaalamu wa afya ya akili atataka kufahamu mandhari-nyuma (feedback) yako na kuhusu magonjwa yoyote makali au matatizo ya hisia ambayo umewahi kuwa nayo zamani.
Watakuuliza kuhusu kipi kilichokuwa kinaendelea maishani kwako hivi karibuni, jinsi sonona ilivyoanza na kama ulishawahi kutibiwa.
Inawezekana wakati mwingine kuwa ngumu kupata majibu ya maswali yote, lakini taarifa utakazotoa zitamsaidia daktari kuweza kukufahamu wewe mwenyewe na kuweza kupata dhana ya chaguo lipi litakuwa zuri kwako.
Kama sonona ni kali au inahitaji matibabu ya kitaalamu, unaweza kuhitaji Kwenda hospitali kupata tiba. Timu inayokupa tiba watahakikisha kuwa unapata tiba na msaada sahihi vitakavyofanya kazi kwako.
Electroconvulsive therapy (ECT)
Electroconvulsive therapy (kwa kifupi ECT) mara nyingi inatumika kutibu:
- Sonona kali kama maisha ya mtu yako hatarini na anahitaji tiba haraka.
- Sonona ya kati au kali kama hakun tiba nyingine yoyote iliyosaidia.
ECT inahusisha kupitisha mkondo wa umeme kupitia ubongo, kwahiyo inatolewa hospitalini kila mara kutumia nusu kaputi. Baadhi ya watu wanapoteza kumbukumbu kwa muda baada ya ECT.
Tiba mbadala
St John’s Wort ni dawa ya mitishamba inayopatikana kwenye maduka ya vyakula vya afya na famasia na inatumika na baadhi ya watu kwa sonona. Kawaida haitolewi au kushauriwa na daktari kwasababu:
- dozi sahihi kwa sonona haieleweki
- aina tofauti zinaweza kutofautiana katika kilichomo
- inaweza kusababisha matatizo makubwa inapotumika na dawa zingine (hasa vidonge vya uzazi wa mpango, dawa inayolainisha mgando au dawa za kifafa)
Ukitaka taarifa Zaidi, ni lazima ujadili na daktari wako.
Ninawezaje kumsaidia mtu mwenye sonona?
- Sikiliza. Hii inaweza kuwa vigumu kuliko inavyosikika. Unaweza ikabidi kusikiliza kitu kile tena na tena. Ni bora zaidi kutokutoa ushauri labda kama umeombwa, hata kama jibu lnaonekan kuwa ni la wazi kabisa. Kama sonona imetokana na tatizo maalum, unaweza kusaidia kutafuat suluhisho au angalau njia ya kutatua tatizo hilo.
- Tumia muda wako nao. Inasaidia japo kuptitisha muda na mtu mwenye sonona. Kuwajulisha kuwa upo pale kwa ajili yao inaweza kusaidia kumhimiza kuongea na kuendelea kufanya vitu vitakavyomsaidia kujisikia vizuri.
- Kuwatuliza. Mtu ambaye ana sonona unapata shida kuamini kuwa anaweza kupata nafuu. Unaweza kuwatuliza kuwa watapata nafuu, ila inawezekana ikabidi urudie tena na tena.
- Msaada wa kujitunza. Hakikisha kuwa wananunua chakula cha kutosha na wanakula mara kwa mara, pamoja na matunda na mboga za kutosha kwenye chakula chao.Unaweza kuwasaidia kutoka nje na kufanya mazoezi kiasi au shughuli zingine wanazofurahia, ambazo ni mbadala na kutumia pombe au madawa ya kulevya kukabiliana na hisia zao.
- Onyesha umakini kwao. Kama wanaterereka na wanaanza kuzungumzia kutokutaka kuwa hai au hata kama wanaashiria kujiumiza, onyesha umakini. Hakikisha kuwa wanamuambia daktari wao.
- Wahimize kukubali msaada. Wahimize kumuona daktari wao, kutumia dawa, au waongee na mtaalamu au mshauri. Kama wana wasiwasi kuhusu matibabu yao, wahimize wajadili na daktari wao.
- Kujitunza mwenyewe. Inaweza kukumaliza kihisia kumpa msaada mtu aliye na sonona, kwahiyo hakikisha unaitunza afya yako ya akili na hali ya utulivu.
Kama una wasiwasi kama mtu yeyote unayemjua anakusudia kujiua
Kuna watu wachache wenye sonona wanaweza kujaribu au kufa kwa kujiua,
Kama una shaka kuhusu mtu yeyote basi ni muhimu kuongea naye kuhusu fikra za kujiua na hisia na uwe makini. Muulize mtu kama ana hisia za kujiua asiweke fikra hizo kichwani mwake au asike kutenda kile anachokifikiria.
Kama bado una wasiwasi kuhusu mtu yeyote, unaweza kuwasiliana na wahudumiaji hapo chini kwa msaada zaidi na ushauri.
Zero Suicide Alliance inatoa mafunzo ya mtandaoni bure kuhusiana na ufahamu na kuzuia kujiua, inatoa mahali pa kuanzia kupata msaada kwa watu ambao wanataka kuwasaidia wale walio na wasiwasi nao.
Kupata msaada kwa ajili ya fikra za kujiua
Kama unahitaji msaada sasa hivi, kuna idara zinazoweza kukusaidia:
Uingereza
Piga simu Samaritans namba 116 123 (simu ya bure), barua pepe jo@samaritans.org au tembelea Samaritans website
Piga simu NHS 111 (simu ya bure) au tembelea kurasa za tovuti ya NHS kuhusu Where to get urgent help for mental health
Wasiliana na daktari wako (Gp) akupe muadi wa dharura (ambao unaweza kufanyika kwa simu au video)
Wasiliana na Local mental health crisis team (kama huifahamu, NHS 111 wanaweza kukusaidia)
Pata msaada mtandaoni kupitia Mind’s I Need Urgent Help web page
Wales
Tembelea Welsh government mental health advice line, ‘C.A.L.L’
(Wales) au piga 0800 132 737 (simu ya bure)
Scotland
Tembelea Breathing Space (Scotland) au piga 0800 83 85 87 (simu ya bure)
Northern Ireland
Tembelea Lifeline au piga 0808 808 8000 (simu ya bure)
Kama unajisikia huwezi kujiweka salama sasa hivi, na msaada mwingine haukutoshi, basi piga 999 au nenda A&E department hospitali ya karibu (wakati mwingine inajulikana kama emergency department). Au, unaweza kumuuliza mtu mwingine apige 999 kwa niaba yako au akupeleke A&E.
Msaada Zaidi
Association of postnatal illness (APNI): APNI inatoa msaada kwa mama wenye sonona baada ya kuzaa. Ipo kuongeza uelewa kwa uma kuhusu hali hii na kuhamasisha utafiti kwenye sababu na asili yake.
Helpline: 0207 386 0868 (10am-2pm Jumatatu hadi Ijumaa)
Black, African and Asian Therapy Network (BAATN): Ni shirika kubwa linalojitegemea, lenye kushughulikia ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa huduma za kisaikolojia kwa watu wenye asili ya weusi, waafrika, waasia ya kusini na watu wa Carribean. Wanatoa taarifa kuhusu afya ya akili, saraka ambayo watu wanaweza kutafuta mtaalamu, matukio, mafunzo na rasilimali zingine. Barua pepe: connect@baatn.org.uk
CALM (Campaign against Living Miserably): Kampeni ya taifa inayozingatia kuishinda sonona na kujiua kati ya vijana wa kiume. Confidential helpline: 0800 58 58 58 (5pm hadi midnight, siku 7 katika wiki)
Depression UK: ni kundi la msaada wa pamoja la kitaifa kwa watu wenye sonona.Email: info@depressionuk.org
Mental health Forum: Jumuiya ya mtandaoni ambapo watu wanaweza kupata msaada wa Pamoja kutoka kwa watu wenye matatizo yanayofanana.
Mind: Ni shirika la hisani la afya ya akili inalotoa ushauri na msaada kwa watu walio na matatizo ya afya ya akili, pamoja na taarifa kuhusu vikundi vya usaidizi maeneo wanayoishi. Helpline: 0300 123 3393 (9am hadi 6pm, jumatatu hadi ijumaa). Pia wanatoa taarifa kuhusu how to cope for people who are supporting someone else. Local Minds wanaweza kukusaidia kutafuta huduma za afya ya akili zinapotolewa karibu na unapoishi.
MindOut: Ni huduma za afya ya akili zinazoendeshwa na kwa ajili ya msagaji, shoga, mwenye jinsia mbili, mtu aliyabadili jinsia na basha (LGBTQ). Wanatoa ushauri na taarifa, msaada mtandaoni, ushauri, kusaidiana na utetezi. Phone: 01273 234 839 Email: info@mindout.org.uk
NHS: taarifa kuhusu jinsi ya kupata huduma za afya ya akili
Papyrus Hopeline UK: nambari za usaidizi zinazotumiwa na wataalamu kutoa ushauri wa utendaji na taarifa kwa watu wenye umri chini ya miaka 35 ambao wanapata fikra za kujiua, au wana wasiwasi kuhusu mtu mwingine. Hopeline: 0800 068 41 41.
Reading well agency: Books on Prescription: Ni mpango unaosaidia watu kumudu ustawi wao kutumia usomaji kujisaidia. Imeidhinishwa na wataalamu wa afya, Pamoja na Royal College of Psychiatrists, na inaungwa mkono na makataba za uma.
Relate: Mtoaji mkubwa wa msaada wa mahusiano Uingereza. Wanatoa huduma mbalimbali za ushauri. Enquiries: 0300 003 0396.
Samaritans: shirika la hisani la kitaifalenye makao Uingereza na Jumuiya ya Ireland linalotoa msaada wa hisia kwa siri kwa mtu yeyote ambaye anajisikia kujiua au mwenye huzuni. Helpline: 116 123. Email: jo@samaritans.org
SaneLine: namba za usaidiza za kitaifa zinazotumika nje ya saa za kazi kutoa msaada wa hisia na taarifa kwa watu waliathirika na matatizo ya afya ya akili. Helpline: 0300 304 700 (4.30 hadi 1.30pm kila siku). Email: support@sane.org.uk
Stonewall: wanatoa taarifa na msaada kwa jumuiya za LGBTQ+, Pamoja na taarifa kuhusu huduma na makundi ya msaada wanapoishi. Freephone: 0800 050 2020 (inafunguliwa Jumatatu had ijumaa, 9.30- 4.30) Email: info@stonewall.org.uk
Switchboard: namba za usaidizi za LGBTQ+ zinazotoa taarifa, msaada na kutoa rufaa kwenda kwa watoa huduma kwa mtu yeyote aliye na hamu ya kuongelea masuala yanayohusiana na ujinsia na/au utambulisho wa jinsia, Pamoja na afya ya akili. Wanatoa online chat, phoneline: 0300 330 0360 (kutoka 10am hadi 10pm kila siku) Email: chris@switchboard.lgbt
Young Minds: shirika la hisani la kitaifa lina;ojitolea kwaboresha afya ya akili ya Watoto wote na vijana wenye umri chini ya miaka 25. Parents’ helpline: 0808 802 5544 (9.30am hadi 4pm Jumatatu hadi ijumaa).
Zero Suicide Alliance inatoa mafunzo ya mtandaoni bure kuhusiana na ufahamu na kuzuia kujiua, inatoa mahali pa kuanzia kupata msaada kwa watu ambao wanataka kuwasaidia watu walio na wasiwasi nao.
Kindly translated by Dr Fii Pendaeli and Dr Nyakomi Adwok, 2022